Na Bertha Lumala
Kocha mkuu wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amewataka wachezaji
wake kuhakikisha wanatikisa nyavu za wapinzani wao BDF XI FC katika
mechi yao ya kesho ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Yanga SC, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, watakuwa na
kibarua kigumu mbele ya wenyeji wao hao watakapopamba katika mechi hiyo
ya marudiano ya hatua ya awali ya michuano itakayochezwa kuanzia saa
2:00 usiku Uwanja wa SSKB Lobatse uliopo Km 70 kutoka Gaborone, mji mkuu
wa Botswana. Uwanja huo upo kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi (BDF) eneo
la Lobatse, Botswana.
Katika mahoajino na mtandao huu akiwa Botswana leo mchana,
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amesema
benchi lao la ufundi linaloongozwa na Pluijm limewataka wachezaji
kuhakikisha wanapata japo goli moja la ugenini huku wakilinda mabao yao
mawili waliyofunga nyumbani.
“Tulishinda 2-0 nyumbani, lakini kocha (Pluijm) amewataka
wachezaji kutobweteka na ushindi huo. Amesema ni lazima tusakae japo
goli moja la ugenini ili tuwe salama zaidi huku tukihakikisha wenyeji
wetu hawapati mabao,” amesema Muro.
Pluijm amesema ushindi wa timu hiyo kwenye mechi za Ligi Kuu ni chachu kuelekea mchezo huo wa marudiano dhidi ya BDF
Aidha, mitandao ya michezo ya Botswana imemnukuu Pluijm akitamba kupata ushindi mwingine wakati timu hizo zitakaporudiana kesho.
Pluijm amekaririwa akieleza kuwa, licha ya kucheza ugenini,
bado ana uhakika watawafunga wenyeji wao BDF XI FC katika mchezo huo.
“Tumekuja Botswana kucheza kwa kushambulia kama tulivyofanya
nyumbani tuliposhinda mabao 2-0, ninajua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu
wanacheza kwao na watataka kutushambulia, lakini sisi tutacheza kwa
malengo huku tukihitaji bao moja ili kuwapa presha wenyeji,” amesema
Pluijm.
Pluijm amesema ushindi wa timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu
Tanzania Bara ni chachu kuelekea mchezo huo wa marudiano dhidi ya BDF na
kuwataka mashabiki kuiunga mkono timu yao kuelekea mechi hiyo.
Hata hivyo, mashabiki wa Yanga SC waliokuwa wasafiri kwa basi
kubwa la klabu hiyo Jumatano alfariji, walikwama kutokana na kile
kilichoripotiwa leo kuwa basi hilo halina bima wala kibali cha
barabarani.
Yanga SC ambayo kwa muda mrefu imekuwa haifiki mbali katika
michuano ya kimataifa ikitolewa kwa matuta dhidin ya Al Ahly ya Misri
katika hatua ya pili mwaka jana, inahitaji sare ya aina yoyote au kipigo
kisichozidi bao 1-0 kusonga mbele.
Endapo timu hiyo ya Jangwani ikifanikiwa kuwang’oa maafande
hao, itakutana na mshindi kati ya Sofapaka FC ya Kenya na Platnum FC
katika hatua inayofuata. Wazimbawe walishinda 2-1 dhidi ya Sofapaka
katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Nairobi wiki mbili zilizopita.
0 maoni:
Chapisha Maoni