
Rais wa Tanzania John Magufuli ametangaza kwamba taifa hilo litanunua ndege zaidi katika juhudi za kufufua shirika la ndege la taifa hilo.
Amesema serikali yake imedhamiria kununua ndege nne zikiwemo ndege kubwa tatu ambazo zitasaidia kuinua "uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini moja kwa moja kutoka nchi zao."
Dkt Magufuli alisema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani, Jim Deboo katika ikulu jijini Dar es Salaam.

Ndege nyingine ambazo Tanzania itazinunua ni ndege moja aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kuwasili Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018.
Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.

"Sisi hapa tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni 2 kwa mwaka, lakini nchi kama Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka, hii yote ni kwa sababu hatuna mashirika ya ndege ya kwetu."
"Kwa hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, unakuta wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza za kwao."
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni